RAIS anayemaliza muda wake nchini Namibia, Hifikepunye Pohamba,
ameshinda tuzo ya Mo Ibrahim inayotolewa kwa kiongozi wa Afrika
aliyeonyesha uongozi bora.Tuzo hiyo yenye thamani ya dola za Marekani milioni tano (sawa na Sh bilioni 9.2 za Tanzania) ni kubwa zaidi duniani kutolewa kwa mtu mmoja mmoja.
Fedha hizo hutolewa kila mwaka kwa kiongozi wa kuchaguliwa aliyetawala vizuri kwa kuinua viwango vya maisha ya raia wake na kisha kuondoka madarakani kwa amani.
Lakini mwaka jana tuzo hiyo ilikuwa ya nne kwa kipindi cha miaka mitano kukosa mshindi.
Pohamba, mpiganaji wa zamani wa waasi aliyepigania uhuru wa nchi yake, alitumikia mihula miwili kama rais wa Namibia.
Alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004, na mara nyingine mwaka 2009. Nafasi yake inatarajiwa kuchukuliwa na Rais mteule, Hage Geingob.
Pohamba alikuwa mwanachama mwanzilishi wa South West Africa People’s Organisation (SWAPO), vuguvugu la msituni lililoendesha harakati za miongo mingi ya kupigania uhuru dhidi ya Afrika Kusini.
Tangu ipate uhuru mwaka 1990, SWAPO imetawala siasa za nchi hiyo ikishinda kwa wingi wa kura katika uchaguzi. Mo Ibrahim ni Mwingereza mwenye asili ya Sudan, mhisani na mfanyabiashara wa sekta ya mawasiliano ambaye alijitengenezea mabilioni ya fedha kwa kuwekeza Afrika.
No comments:
Post a Comment