Mtwara. Waziri wa Ujenzi na mgombea urais wa
CCM, Dk John Magufuli amesema kuwa wana-CCM mwaka huu wanapaswa kufanya
kampeni za kisayansi zaidi kuhakikisha wanapata ushindi wa tsunami
utakaowezesha kuundwa kwa Serikali imara itakayowaletea maendeleo
Watanzania wote.
Alisema kwa kufanya hivyo kutawasaidia
kupata viti vingi na kusimamia shughuli zote za maendeleo na kwa
manufaa ya wanaCCM na Watanzania wote kwani mahitaji yao na matarajio
yao ni kupata maendeleo makubwa.
“Niwaombe wana CCM
wenzangu, tushikamane tuwe wamoja. Kampeni za mwaka huu ni lazima
tufanye kampeni za kisayansi zaidi, ni lazima kampeni zianze katika
ngazi ya nyumba kumi, vitongoji kwa vitongoji, vijiji, mitaa, kata
majimbo , wilaya, mikoa na baadaye urais kwa ujumla. Katika umoja huu
nataka niwahakikishie ushindi wa mwaka huu wala si wa kimbunga, ni wa
tsunami,” alisema Dk Magufuli.
Dk Magufuli aliyekuwa
katika ziara ya mikoa ya kusini ya kuzindua miradi mbalimbali ya
maendeleo iliyotelekezwa katika kipindi cha awamu ya nne ya Rais Jakaya
Kikwete, alisema hayo hapo jana wakati akizungumza na wanachama wa chama
hicho nje ya ofisi za CCM mkoa wa Mtwara, ikiwa ni siku moja baada ya
rais kukamilisha ziara yake na kuwaaga wananchi wa mkoa huo.
Mgombea
huyo na mbunge wa Chato alibainisha kuwa amekuwa kiongozi katika maeneo
mbalimbali nchini kwa kipindi kirefu, hivyo anakifahamu vema chama,
shida za wanaCCM na matarajio yao yanayojumuisha matarajio ya Watanzania
wote na shida zao.
Alisema kuwa endapo atachaguliwa
kuwa rais, hatawasahau wanaCCM na Wanamtwara kwa ujumla, lakini wote hao
wanapaswa kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa kuwa maendeleo hayana
chama na akichaguliwa atakuwa rais wa Watanzania wote.
Alisema
katika kipindi cha miaka 20 ya uongozi, amekuwa akifika Mtwara na hivyo
ana uhakika endapo Wanamtwara wataamua kumpatia nafasi ataujua zaidi
mkoa huo kuuendeleza katika kipindi cha miaka mingine zaidi.
“Wanamtwara
nafahamu matarajio yenu, nataka niahidi kwenu na nimwombe Mungu
nitapenda sana niwe mtumishi wa watu, nisiwe na majivuno wala kujiona,
niwe mtumishi hasa wa wanyonge niweze kuwasikiliza na kusikiliza
matarajio yao.
“Matarajio ya Watanzania na Wanamtwara
ni makubwa, wanahitaji maendeleo makubwa na tunahitaji kuyasukuma. Nchi
yetu imelelewa katika misingi ya umoja pasipo kubaguana kutokana na
maeneo tunayotoka, dini, makabila hivyo tunahitaji umoja na palipo na
umoja pana amani na palipo na amani pana maendeleo,” alisema Dk
Magufuli.
Makundi ndani ya vyama
Akizungumzia
makundi katika chama hicho, alisema yalikuwapo zaidi ya 40 na baada ya
uchaguzi makundi yote yalimuunga mkono yeye aliyepitishwa na vikao vya
chama, hivyo wanaoondoka ndani ya chama hicho kwa chama kikubwa kama CCM
ni jambo la kawaida kwa kuwa hata enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere wapo walioondoka na waliofukuzwa.
“Mti ambao
unataka upate mbao zake nzuri, matawi kudondoka ni neema, lakini kwa
watu kuondoka ndani ya CCM ni kawaida na kwa chama kikubwa kama CCM ni
jambo la kawaida sana,” alisema Dk Magufuli.
Mtwara wajipanga
Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Mtwara, Homamed Sinani alisema watahakikisha CCM Mtwara
inaendelea kupata ushindi wa kishindo kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge
na urais.
“Chama kipo imara, mimi kama mwenyekiti wa
chama mkoa nasema chama kimejipanga kikamilifu na nina imani kama
mshikamano ukidumishwa tunatarajia ushindi wa vishindo kuanzia ngazi ya
udiwani, ubunge hadi urais,” alisema Sinani.
JK akemea siasa chafu
Katika
hatua nyingine, wakati akihitimisha ziara yake juzi, Rais Kikwete
aliwataka wanasiasa mkoani Mtwara kuacha siasa chafu za kupotosha
wananchi badala yake wawaambie ukweli juu ya miradi na mikakati ya
maendeleo inayoendelea mkoani humo.
Rais Kikwete alitoa
kauli hiyo juzi wakati akiweka jiwe la msingi katika tawi la Benki Kuu
ya Tanzania (BoT) tawi la Mtwara ambalo ni la saba nchini na baadaye
kuirudia wakati akihutubia mkutano wa kuwaaga wananchi.
Rais Kikwete aliwataka wananchi kutosikiliza maneno ya watu wapotoshaji wanaotafuta umaarufu wa kisiasa kwa bei nafuu.
Alisema kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kuzuia maendeleo ya Mtwara kwa sababu kuna fursa nyingi zinazovutia uwekezaji.
“Msisikilize
maneno ya wapotoshaji wanaotafuta umaarufu wa kisiasa kwa bei nafuu,
Mtwara na Lindi kulichelewa lakini kutakuwa kwa kwanza na kule
kulipokuwa kumetangulia kutafuata,” alisema Rais Kikwete.
Ingawa
hakufafanua, kauli hiyo ya Rais Kikwete ilikuwa inalenga vurugu za
wananchi wa Mkoa wa Mtwara zilizotokea mwaka jana zikipinga usafirishaji
wa gesi kwa njia ya bomba kwenda Dar es Salaam ambazo zilihusishwa na
ushawishi wa kisiasa.
Hata hivyo alisema kuwa Mtwara
ndio muhimili mpya wa uchumi wa Tanzania kutokana na kuwa na rasilimali
nyingi zinazotoa fursa za uwekezaji hivyo kunahitajika uwepo wa huduma
za kibenki kwa karibu.
“Wanasiasa wa Mtwara
msiwachanganye wananchi badala ya kuwaeleza msimamo sahihi wenye
mwelekeo mnakwenda kuwapeleka kwenye mambo ambayo yanawaongezea sifa ya
muda mfupi na kuwavuruga wananchi hawa na kukosa utulivu wa kufanya
mambo ya maana,”alisema Rais Kikwete.
haha ha
ReplyDelete