Dar es Salaam. Mgombea urais kwa tiketi ya
Chadema anayewakilisha vyama vinavyounda Ukawa, Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa amesema maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsindikiza
wakati akienda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu ni salamu
kwa CCM na ‘wameisoma namba’ kwamba Watanzania wanataka mabadiliko.
Akiwahutubia
mamia ya wafuasi wa vyama vinavyounga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) katika Ofisi za Makao Makuu ya Chadema jana, Lowassa
aliyeonekana kuwa na furaha muda wote, alisema maandamano waliyoyafanya
hayajawahi kutokea katika historia ya Tanzania.
“Haijatokea
katika historia ya nchi yetu maandamano makubwa ya aina ile,
nimefurahishwa na vijana wametembea kutoka Buguruni hadi Kinondoni na
hamjachoka nawapongeza sana, asante sana,” alisema Lowassa.
Alisema
ana mambo mawili ya kusema; kwanza kuwashukuru wafuasi na wapenzi wa
Ukawa kwamba kwa kujitokeza kwa wingi wamepeleka meseji moja kwa
wasiowatakia mema, wanaosema CUF na Chadema ni watu wenye fujo,
wamethibitisha kwamba si kweli.
“Tumewahakikishia kuwa
sisi ni watu wenye nidhamu na uwezo, Mwenyezi Mungu akipenda Oktoba
tunachukua nchi asubuhi peupeee, kwa hiyo watu wasitafute visingizio,
watafute vingine, watoto wa mjini wanasema wameisoma namba,” alisema
Lowassa huku akishangiliwa na umati wa watu.
Akizungumzia
jambo la pili, mbunge huyo wa Monduli aliyejiondoa CCM siku 15
zilizopita, alisema anauchukia umaskini kiasi kwamba anauona kama ukoma.
Lowassa
ambaye mara nyingi husema hajakutana barabarani na Rais Jakaya Kikwete,
alisema rafiki yake huyo ndiye aliyeharibu uchumi wa nchi, lakini
akasema asingetaka kutoa mashtaki bali kutoa takwimu za hali
ilivyobadilika.
“Wakati Rais Benjamini Mkapa anaondoka
madarakani, bei ya sukari ilikuwa Sh650, leo ni Sh2,300, kutoka 650 hadi
2,300 ameharibu uchumi, hajaharibu?” aliuliza na kujibiwa,
“ameharibuuu.”
“Bei ya mchele ilikuwa Sh550 leo
Sh2,200, ameharibu uchumi, hakuharibu? Sembe kilo ilikuwa Sh250 leo ni
Sh1,200, ameharibu hakuharibu?” alihoji Lowassa na watu wakamjibu
‘ameharibuuu” na kisha akaongeza kuwa kwa sababu hizo, CCM haistahili
kuendelea kutawala.
Lowassa alitumia fursa hiyo
kuwaalika wanachama wa CCM wasioridhika na hali ilivyo kujiunga na Ukawa
kwa kuwa inawezekana kutafuta mabadiliko nje ya chama hicho na kwamba
wasione haya bali waangalie idadi kubwa ya vijana waliojitokeza jana.
Mgombea
huyo, alisema Tanzania imeshuhudia uporaji mkubwa wa mali za Taifa,
ambapo tembo wameuawa kuliko wakati mwingine wowote, hivyo kutokana na
vitendo hivyo, CCM haistahili kuendelea kutawala.
Kuhusu
kutunza shahada za kupigia kura, Lowassa alisema Wanaukawa hawapaswi
kufanya mchezo kwa kuwa CCM imekuwapo madarakani muda mrefu watatumia
kila kitu ndani ya uwezo wao kubaki madarakani.
“Na
sisi tutumie kila kitu kilicho ndani ya uwezo wetu kuingia madarakani.
Kitakachotuingiza madarakani ni kura, hifadhi shahada yako, shawishi na
wengine, tarehe 25 Oktoba tunawatoa madarakani,” alisema.
Alisema
amesikia maneno kuwa kuna mchezo wa watu wanapita mitaani wanachukua
shahada za kupigia kura za wanajeshi, askari magereza wanachukua namba.
Alimuhoji
mmoja wa wanasheria wa Chadema, Mabere Marando iwapo kama amesikia
taarifa hizo, naye akajibu: “Kwa niaba ya wanasheria wote wa Chadema
tunaahidi kitu kimoja, njama zote walizonazo kujaribu kuhujumu kura za
Lowassa tutazidhibiti, njama zote walizonazo kuhujumu ushindi wa wabunge
wetu tutazidhibiti, njama zote walizonazo kujaribu kudhibiti ushindi wa
madiwani tutazidhibiti.”
Marando alisema mawakala wote
wa vyama hivyo wanapaswa kupeleka matokeo ya vituo vyote baada ya
kubandikwa saa 12 jioni na kwamba yeye hatasubiri atatangaza badala ya
kusubiri saa saba usiku.
Mbatia
Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi na mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema
maandamano yaliyofanyika jana ni historia mpya ambayo ni elimu kwa
Watanzania. Ari iliyoonyeshwa tangu asubuhi inasadifu hamu ya
Watanzania.
Pia, alisema Rais Kikwete ametangaza kuwa
wapinzani ni maadui na kumtaka kuangalia lugha anayoitumia, kwa kuwa
Ukawa watajibu kwa hoja na si matusi.
“Ninamhusia sana
Rais Jakaya Kikwete amebaki na siku 75 tu za kuwa Amiri Jeshi Mkuu, ni
ushauri wangu wa bure kabisa yeye na wenzake wachunge sana ndimi zao,
maslahi ya taifa kwanza vyama baadaye, tunampa nishani iwapo atamaliza
siku 75 kwa amani na kumkabidhi Amri Jeshi Mkuu, Edward Lowassa,”
alisema Mbatia. “Rafiki yangu (Ibrahimu)Lipumba amekimbia akidhani Ukawa
utaparaganyika lakini sasa umeimarika zaidi,” alisema Mbatia huku
akishangaliwa na umati wa watu na kumaliza kuwa “Hakuna mwanadamu ambaye
yupo juu kuliko wengine au taasisi yoyote.”
Makaidi
Mwenyekiti
wa NLD Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi alisema kuwa
katika umri wake mkubwa alionao hajawahi kuona maandamano ya watu wengi
kama waliojitokeza kumsindikiza Lowassa jana.
“Nina
miaka 74 lakini sijaona kitu kama cha leo nakaanza kujiuliza hii maana
yake nini? Nikachukua mfano kama mimi ni chama tawala na wapinzani ni
wengi namna hii ningeanza kufanya nini, ningejiuzulu mara moja,” alisema
Makaidi.
Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha Tasilima
alisema kuwa walioleta siasa mbaya nchini wanatakiwa kuwajibika kwa kuwa
wamesababisha kuwapo kwa uchumi mbaya pia.
“Lowassa akiingia Ikulu ataenda kuondoa uchumi na siasa mbaya,” alisema Tasilima.
Maalimu Seif
Katibu
Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alisema umati mkubwa wa vijana
waliojitokeza kumsindikiza Lowassa umedhihirisha kuwa watu walikuwa
wamekata tamaa sasa wanataka matumaini mapya.
Hata
hivyo, alisema haitoshi kumsindikiza Lowassa kwa idadi kubwa namna hiyo
kama hawataenda kupiga kura kwa kuwa maandamano hayawezi kuiondoa CCM
madarakani.
“Hatutaishinda CCM kwa maandamano bali kwa kupiga kura, tunza kadi yako zimebaki siku chache,” alisema Hamad.
Onesmo Ole Nangolo
Aliyekuwa
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole, alipokewa rasmi
na kusema alijiunga CCM mwaka 1977, lakini alichokishuhudia Dodoma
kwenye uchaguzi wa mgombea wa Rais kwa tiketi ya chama hicho
kimemlazimisha kuhamia Chadema.
“Ile CCM niliyokuwa
naifahamu si tuliyokwenda juzi Dodoma, misingi na haki imegeuka,
kimekuwa chama cha viongozi wachache kwa maslahi yao binafsi,
unyanyasaji umetawala ndani ya CCM, sina moyo wa chuma, sikuridhika na
mchakato wa Dodoma,” alisema Nangolo.
Ilivyokuwa
Jiji la Dar es Salaam lilisimama kwa wastani wa saa nane kutokana na msafara wa Lowassa kwenda kuchukua fomu.
Makundi
ya watu wa kada mbalimbali wakiwamo madereva wa bodaboda, bajaji,
magari na watembea kwa miguu walionekana kufunga barabara ya Uhuru
kuanzia Buguruni eneo la Rozana zilipo ofisi za CUF na Posta zilipo
ofisi za NEC.
Maandamano hayo yalisababisha msongamano
wa magari na kusababisha magari ya abiria maarufu kama daladala na
magari binafsi kutafuta njia mbadala kufanikisha safari zao.
Idadi
ya watu waliojitokeza katika msafara inaweza kufananishwa na ile
iliyojitokeza wakati wa ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama Julai
2013.
Watu wengi walionekana wakitumia simu kupiga
picha na kurekodi video za matukio mbalimbali pembeni mwa barabara huku
wengine wakiwa juu ya maghorofa wakitazama.
Wapo
waliokuwa wakitoka maofisini na kukaa pembezoni mwa barabara kushuhudia
tukio hilo huku maelfu wakitembea umbali wa kilometa sita kuufuata
msafara huo.
Msafara huo ulitumia saa mbili na nusu kutoka Buguruni hadi ofisi za NEC.
Kabla ya msafara
Wafuasi
wa vyama vinavyounda Ukawa; CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD walianza
kukusanyika tangu saa moja asubuhi katika makao makuu ya CUF yaliyopo
Buguruni na viongozi mbalimbali walianza kuingia saa 3:56 asubuhi na
kumkuta mwenyeji wao Maalimu Seif.
Wengine
Makundi
ya mashabiki waliokuwa wakizunguka wakiimba nyimbo mbalimbali, ukiwamo;
‘kama siyo juhudi zako Kikwete, Lowassa tungempata wapi? Na wengine
wakikejeli, “Magufuli toroka uje, Tanzania mpya bila CCM inawezekana,
tumechoka kuokota makopo na funguo za Magufuli zipo Ukawa.
Safari ya Biafra
Baada
ya kukabidhiwa fomu na Ofisa Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), Deogratius Nsanzugwanko, Lowassa, mgombea mwenza, Juma Duni Haji
na viongozi waandamizi wa Ukawa waliendeleza msafara wa kwenda Makao
Makuu ya Chadema mtaa wa Ufipa, Kinondoni.
Licha ya
umati uliomsindikiza kutembea kilomita nane ukitoka Buguruni, idadi ya
watu ilizidi kuongezeka na kuendeleza maandamano yaliyoanzia makutano ya
mtaa wa Ghana na Ohio ilipo NEC kupitia Barabara ya Barack Obama na
kuunga hadi Ali Hassan Mwinyi.
Kama ilivyokuwa awali,
wafuasi hao waliendelea kuimba bila kuchoka nyimbo mbalimbali za hamasa
ili wasichoke na kila eneo walilokuwa wakipita umati mkubwa wa watu
waliojipanga katika barabara hizo ulishangilia na hata kuwafanya baadhi
ya waliokuwamo kwenye magari kuonyesha alama ya “V” inayoyotumika na
Chadema.
Msafara ulizidi kuongezeka urefu baada ya wale
waliochelewa kuungana nao na baadaye uliiacha barabara ya Ali Hassan
Mwinyi na kuingia barabara ya Kinondoni ambayo kutokana na wembamba wake
iliwalazimu wenye magari waliokuwa safarini kuegesha pembeni kupisha
watu waliokuwa wakiandamana.
Katika safari yote hiyo,
polisi walikuwa wameegesha magari yao katika kila umbali wa kilomita
moja na nusu au zaidi na kufanya umati huo uwashangilie kila
unapowapita.
Licha ya kuwa taarifa za awali
zilibainisha kuwa maandamano hayo yangeishia Makao Makuu ya Chadema,
ilibidi uongozi wa chama hicho ubadilishe utaratibu na kuwapeleka watu
wote katika Viwanja vya Biafra, Kinondoni kwa kuwa eneo la mtaa wa Ufipa
lisingetosha.
Walipofika Biafra baada ya kumaliza
takribani kilomita saba kutoka NEC, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum
Mwalimu aliwasalimia wafuasi hao na kumkaribisha Lowassa awashukuru
ambaye alizungumza kwa ufupi akitamka maneno, “hii haijawahi kutokea.”
Lowassa
aliwapongeza polisi kwa kufanya kazi kwa weledi na kueleza kuwa busara
na amani vilivyotumika katika maandamano hayo vinadhihirisha kuwa
Chadema na Ukawa ni vyama vya kushika dola.
Baada ya
watu kutawanyika, msafara wa viongozi ulirudi mtaa wa Ufipa kuendeleza
hotuba ambako baadhi ya wafuasi walioshtukia kuwa walidanganywa walirudi
kwenda kuwasilikiliza viongozi.

No comments:
Post a Comment