![]() | |
| Kiongozi wa UVCCM |
Wakati joto la urais likizidi kupanda ndani ya CCM kutokana na hofu ya baadhi ya majina mazito ya wagombea wa nafasi hiyo kukatwa kwa mizengwe, vita vya wagombea sasa ni dhahiri baada ya mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kusema hakuna mtu atakayekatwa bila ya sababu za msingi.
Mjumbe huyo, Sadifa Juma Hamisi, ambaye ni
mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), pia alisema umoja huo
haujafikia uamuzi wala kumtuma mtu kumdhibiti mwanachama anayetajwa
kuwania urais.
Katika siku za karibuni kumekuwapo mjadala mkubwa
ndani ya CCM juu ya mtu atakayepitishwa kuwania urais kwa tiketi ya
chama hicho, na ilizidi baada ya Rais Jakaya Kikwete kueleza kuwa
mwanachama ambaye atateuliwa na CCM kugombea urais hayumo miongoni mwa
waliojitokeza na kuwataka wanachama kuwashawishi watu wenye sifa
wajitokeze.
Siku chache baadaye, Dk Raphael Chegeni aliliambia
gazeti la Mwananchi kuwa ametumwa na wanachama wa CCM wa mikoa ya Kanda
ya Ziwa kwenda kumshawishi Lowassa kujitokeza kuwania urais kuitikia
wito wa Rais Kikwete wa kuwataka wanachama kuwashawishi watu wenye sifa
kujitokeza.
Hadi sasa, wanachama waliojitokeza kuwania
kuteuliwa na CCM kugombea urais ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, January
Makamba (Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia), Hamisi Kigwangala, na
Lazaro Nyalandu ambaye ni waziri wa Maliasili na Utalii.
Lakini pia wako wanaotajwa kuwania urais lakini
hawajatangaza ambao ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel
Sita, William Ngeleja, Emmanuel Nchimbi, Mwigulu Nchemba, Stephen
Wasira, Bernard Membe na Edward Lowassa ambaye ameibua mjadala kati ya
kambi yake na zinazompinga.
Mapema wiki iliyopita, katibu wa uhamasishaji na
chipukizi wa UVCCM, Paul Makonda alikaririwa akisema kuwa vitendo vyake
vya kumshambulia Lowassa vinatokana na kutumwa na umoja huo kumdhibiti,
jambo ambalo limezidisha mjadala kuhusu mteule wa chama hicho.
Kutokana na hofu hiyo, viongozi wa UVCCM na CCM
mkoani Arusha wametuma ujumbe wa maneno kwa Kamati Kuu na Halmashauri
Kuu ya Taifa za chama hicho wakitaka wanachama wasifanyiwe kile
wanachokiita kuchafuana na vitisho vya baadhi ya wagombea kukatwa
kimizengwe.
Ujumbe huo ulitumwa juzi na mwenyekiti wa CCM wa
mkoa, Onesmo ole Nangole na mwenyekiti wa UVCCM, Robinson Meitinyiku
ambao walitaka Sadifa Juma Hamis kueleza msimamo wa mkoa kwa vyombo
hivyo viwili vya maamuzi, na mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM
aliwahakikishia kuwa hakuna mgombea atakayekatwa kwa “sababu za
kijinga”.
Akijibu ujumbe wa viongozi hao, Sadifa aliyekuwa
jijini hapa kumsimika kamanda wa vijana wa wilaya ya Arumeru, Mathias
Manga, aliwaondolea hofu katika hafla hiyo akisema hakuna mgombea wa
urais wa CCM ambaye atakatwa bila sababu za msingi, lakini akawataka
vijana kusubiri zamu yao hadi 2025.

No comments:
Post a Comment